Mwanakontenti wa habari za burudani mtandaoni, Mungai Eve, amejitokeza na ombi la msamaha kwa msanii na mjasiriamali Esther Akoth, akidai kuwa amechapisha taarifa za kumharibia jina. Mungai Eve alitoa ombi hilo kupitia ukurasa wake rasmi wa Facebook na kujutia kuchapisha habari za kupotosha kuhusu msimamo wa msanii maarufu, Akothee, katika masuala ya ndoa.
Katika taarifa yake, Mungai Eve alikiri makosa yao na kuahidi kuwa makini zaidi katika kuchapisha habari ili kuhakikisha zinakuwa za uhakika na za kuaminika. Hatua hii inajiri wakati Akothee, anayejulikana pia kama Madam Boss, akitishia kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wanahabari wa kidigitali wanaotumia habari zake kwa lengo la kuvutia wafuasi.
Madam Boss alisisitiza kuwa baadhi ya bloga wanajikita zaidi katika kutangaza matatizo ya maisha yake na kupuuza mafanikio yake na kazi yake. Aliwataka wanahabari hao kuacha kutumia jina lake bila idhini na kuonya kuwa watalazimika kulipa faini ya Shilingi 300 milioni iwapo wataposti chochote kinachomharibia jina.
Hata hivyo, haikubainika wazi ni nini hasa kilichosababisha Mungai Eve kuomba msamaha kwa Akothee, na hii ilisababisha mashabiki kumshambulia mitandaoni wakidai kuwa anatafuta umaarufu mitandaoni.
Kufikia sasa, hakuna majibu kutoka kwa Mungai Eve kuhusu masuala haya, na baadhi ya watu mitandaoni wamehoji ukweli wa ombi la msamaha huku wakidai kuwa habari hiyo haikuwa na nembo, sahihi, au muhuri wa kuthibitisha uhalali wake. Vilevile, kumekuwa na maoni tofauti kuhusu ukweli wa habari hiyo, na baadhi ya watu wakihitaji uthibitisho wa taarifa zilizochapishwa.
Kwa upande mwingine, madai ya mfarakano kati ya Akothee na mume wake Mswizi, Denis Schweizer, aliyejulikana kwa jina la utani ‘Omosh’, bado yanabaki kuwa mjadala mkubwa, na taarifa kamili za tofauti hizo bado hazijulikani hadi sasa. Akothee ameshindwa kutoa ufafanuzi kuhusu kinachoendelea katika ndoa yao iliyofungwa rasmi kupitia harusi ya kisasa mnamo Aprili 2023.