Bizzare

Tana River: Wanawake washtuka kugundua waume wao kumbe ni mashoga!

WANAWAKE wawili katika Kaunti ya Tana River walipata mshtuko mkubwa, baada ya kugundua kwamba waume wao ambao wamekuwa marafiki wakubwa kwa muda, wamekuwa wakichumbiana.

Mke wa afisa wa mikopo katika benki moja maarufu nchini na mwenzake aliyeolewa na mchuuzi wa bidhaa za kuku, walipata habari hiyo baada ya picha ya wanaume hao wawili kuibuka kwenye mitandao ya kijamii wakibusiana.

Katika picha hiyo iliyotokea kwa bahati mbaya kwenye hadhi ya WhatsApp ya mchuuzi husika, wawili hao wanaonekana wakijaribu kupigana busu wakiwa nusu uchi, na maandishi chini yake yakisema “Happy Valentine’s My Sweetheart in Advance.”

Hata hivyo, imeibuka kuwa uhusiano kati ya wawili hao ulianza kitambo, na wawili hao wamekuwa pamoja mara kadhaa sehemu tofauti tofauti kila walipopata nafasi.

Rafiki wa karibu wa wawili hao aliekeza kwamba wawili hao walienda likizo ya wapendanao huko Copa Cabana eneo la Mtwapa, wakiwaacha wake zao bila taarifa muafaka.

“Wake zao wamekuwa wakifikiri kuwa ni marafiki wazuri sana kwa vile yule jamaa mchuuzi ni mshiriki anayejitolea sana kanisani, hata alifunga ndoa takatifu na mke wake humo,” alisema rafiki huyo.

Kulingana na marafiki wa mke wa mchuuzi, mumewe alimuaga kuwa alikuwa anaenda kutafuta muuzaji wa bei nafuu eneo la Mtwapa, Kaunti ya Kilifi. Aliahidi kurejea baada ya siku chache. Naye mfanyakazi wa benki alikuwa likizo na alikuwa katika safari ya kurejea kazini wiki ijayo kutoka bara.

“Likizo yake ilikuwa imalizike wiki ijayo. Sisi vile vile tumeshtushwa na taarifa hizo kwa sababu hafanani na tukio hilo kabisa. Hatujawahi kufikiria,” alisema mwenzake.

Ni tukio ambalo limewasababishia wanawake hao wawili huzuni, kwani sasa ndio gumzo la mjini.

Mke wa mchuuzi inasemekana ametoroka mji wa Hola ili kuepuka aibu hiyo mitaani. Mumewe, ambaye ni mke katika uhusiano na mfanyakazi wa benki, naye ameripotiwa kupanda basi Jumamosi alfajiri. Mchumba wake anayefanya kazi benki bado hajaonekana mjini Hola.

Waumini wa kanisa wanalohudhuria wamebaki vinywa wazi pia.

“Shetani ni mwongo, huyo mchuuzi huwa na ukaribu sana na mchungaji na huwa ni mtu wa kujituma sana kanisani, namhurumia mke wake. Inasikitisha sana lakini tunaendelea kuomba,” alisema Anna Mugambi, muumini wa kanisa hilo.

Juhudi za kuwatafuta wake hao ili watoe maoni yao hazikuzaa matunda kwani simu zao zilisalia kuzimwa.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wachungaji na Maimamu Mchungaji Robert Mkolwe anabainisha kuwa uhusiano wa watu wa jinsia moja unazidi kuongezeka katika kaunti hiyo hivyo basi haja ya wazazi kuwa waangalifu.

“Unaweza kuona sasa ndoa zinasambaratika. Ipo haja ya kuomba na kuwashirikisha washiriki wa kanisa letu. La sivyo tutapoteza jamii,” alieleza.