''Ninapokuwa karibu na mwanaume ninaishiwa na nguvu'' Jacinta Wambui -
gossips

”Ninapokuwa karibu na mwanaume ninaishiwa na nguvu” Jacinta Wambui

Hisia zake na mawazo yake pamoja na upeo wake hususani kuhusu jinsia ya kiume au wanaume kwa ujumla, ni tofauti mno na ile ya wanawake wengi wa rika lake .

Jacinta amejitokeza wazi wazi kuzungumzia hali hii ambayo imegubikwa na wasiwasi mkuu anaoishi nao kila siku anapowakaribia wanaume au hata kuwa karibu na wao .

Sasa inakuwaje wakati anakaribiwa na mwanaume?

Jacinta anakiri kuwa hilo linapofanyika na kwakuwa hawezi kujizuia hali hiyo hujitokeza , hukumbwa na uoga usiokuwa wa kawaida .

Jacinta amekiri kuwa hali aliyonayo ni ya kisaikolojia na pia ni ugonjwa wa kiakili, ni hali ambayo amepambana nayo tangu akiwa binti mdogo .

“Wakati mwingine mimi huwaza nitawezaje kubeba bango , ambalo limeandikwa sitaki kuzungumza na mtu , kwani kila mahali ninapokwenda wengi huniuliza ni kwanini mimi huwa mkimya? Na bila shaka hali ninayo ipitia ni ngumu sana tena sana “Jecinta anasema.

Ulimwengu wa hofu

Kuanzia pale alipoanza kujitokeza kwenye baadhi ya mitandao ya kijamii nchini Kenya, ili kuzungumzia hali yake anasema kuwa imemgharimu ujasiri mwingi. Lakini anasema kuwa hata wakati anajitokeza huwa anajawa na wasiwasi mkubwa na mawazo kuhusu watu wanamuwazia vipi na wanamchukuliaje?

Jacinta amekiri kuwa anaishi na hali ambayo inajulikana kitaalamu ‘anthrophobia ‘ ikitafsiriwa na wataalamu wa magonjwa ya kiakili kama hofu ya watu au kitu kingine chochote .Hali kadhalika Jacinta anakiri kuwa ana changamoto ya kutangamana na watu , kama watu wengine kwa mfano yeye huhisi ni vigumu kuanza mawasiliano na watu au kushiriki mazungumzo ya aina yoyote.

“Unajua kuna tofauti ya kuwa mtu mwenye aibu na kuwa na hali kama ninayoishi nayo ya kutopenda kuchangamana .Kuona hayo ni wakati unahisi wasiwasi kidogo tu wakati uko karibu na watu wengine , ila hali kama hii ninayoishi nayo mtu huwa ana uoga na kujiuliza maswali mengi ya ‘je’ …..

Jacinta Wambui

Mwanadada huyu anasema kuwa haya yameathiri sana maisha yake mno kwani yeye huwa hataki kabisa kuwa katika maeneo ambayo kuna mikusanyiko ya watu . Vilevile wakati ambao pengine hawezi kuepuka kuwa miongoni mwa watu anasema kuwa mwili wake huanza kutetemeka na roho yake kudunda kwa mwendo wa kasi usio wa kawaida . Vile vile akiwa sehemu ambayo ameshindwa kuwa pekee yake anahisi kana kwamba anatokwa na kijasho chembamba asijue la kufanya .

“Maisha yangu yamekuwa na upweke mwingi , kwani hata sasa siwezi hata kuchumbiwa au hata kuitwa miongoni mwa wanarika kama mimi kutokana na hofu ambayo hunizingira .

Kwa mfano ni vigumu mno kwangu kula wakati watu wananitazama , kila wakati huwa ninahisi uoga hata kuingia kwenye mgahawa na kula huku watu wakiniangalia . Ikiwa itanilazimu niingie kwenye mgahawa huwa nitatafuta sehemu ambayo nitaangalia ukuta “Jacinta anasema

Je ni kwanini anawaogopa wanaume wote .

“Uoga ambao ninao dhidi ya wanaume umeniathiri mno , kwa kiwango kuwa kwa umri nilionao kwa sasa wa miaka 24 sijawahi kutoka na hata rafiki wa kiume , sijawahi kuchumbiwa , na nimeanza kujiuliza sasa nitaishije hivi nikiwa peke yangu”? anasema Jacinta

Mwanadada huyu anakiri kuwa sio kwamba hafuatiliwi na jinsia ya kiume, shida huwa hatua hiyo inapojitokeza yeye huwa na haraka kuwakwepa .

“Ninaweza kuhesabu hata wanaume kati ya 15 hadi 20 ambao walinifuatilia wakitaka mahusiano nami ila wanaponikaribia mimi huwakwepa kwa haraka – baadhi yao wanafikiria kwamba mimi ninaona haya , ila mimi ni na shida kubwa ya kuwaogopa wanaume wote .

”Ninapokuwa karibu na mwanaume huwa ninahisi kana kwamba ninaishiwa na nguvu na kinachofuata ni kutafuta njia ya kuondoka .”Anasema Jacinta

Ni hali ambayo sio ya kawaida ambayo mwanadada huyu anasema kuwa hata wananaume walioko kwenye jamii yake kwa mfano , binamu zake na wajomba wake huwa hataki kuwa karibu nao.

Pia hajawahi kuwa na rafiki mwanaume katika maisha yake yote hata wale ambao anafanya nao kazi

“Nina picha moja ambayo nilipigwa nikiwa mtoto wa miaka 3 ambapo mtoto wa kiume amesimama kando yangu , ila mimi ninaonekana nikilia , huwa ninamuuliza mama yangu ni kwanini nilikuwa ninalia , mama anasema kuwa ni kwasababu nilikuwa nimesimama kando ya mtoto wa kiume , na kwa hiyo ninapoangalia maisha yangu ya utotoni huwa ninawazia binti ambaye hakupata usaidizi wa kiakili na wa kisaikolojia wakati ilipohitajika .”anasema Jacinta.

“Hali hii yote Inatokana na unyanyasaji. Huwa naona wanaume kama tishio, ni kana kwamba akili yangu imekuwa ikiwaona wanaume kama tishio , na wenye uwezo wa kunifanyia mabaya .

Hata ninapochangamana nao najisikia kujitenga kabisa na wao . Siwezi kuzungumza nao kwa muda mrefu , na kwa hiyo ninahisi kana kwamba siwezi kuwa na mazungumzo ya kawaida nao kwa muda mrefu, nitakuwepo kimwili kama mwanaume anazungumza nami lakini akili yangu iko mbali”. Anasema Jacinta.

Jacinta anasema kuwa wakati yuko binti mdogo hakufahamu kuwa kidonda cha dhuluma ya kingono iliyotendeka utotoni kingekuwa na athari kuu katika maisha yake ya usoni.

Ila anasema kuwa kila wakati alikuwa anajiuliza basi ni vipi yeye huogopa wanaume namna hiyo ? kwa sababu anafikiria kuwa hapawezi kuwa mtu wa kawaida awe mwanamke au mwanaume awe na uwezo wa kuogopa jinsia nyingine namna hiyo.

Japo hajataka kuzungumzia kwa kina kirefu tukio la ubakaji akiwa mtoto mdogo – anasema kuwa wakati huo hakupata usaidizi uliohitajika wa kumuwezesha kuendelea na maisha ya kawaida.

Na sasa anaona kwamba kule kunyamaziwa kwa tukio hilo kumekuwa na athari nzito za kisaikolojia katika maisha yake

“Shuleni pia nilikuwa mpweke mno , na nilikuwa sina marafiki .Darasani nilikuwa sizungumzi hata kidogo. ,Nilikuwa nina hofu ya kunyoosha mkono wangu kuuliza maswali au kujibu maswali kutoka kwa mwalimu.

jacinta Wambui

”Nakumbuka kuwa kulikuwa na mwalimu mmoja aliyeniita neno ‘mayai’ kwani huyu mwalimu alikuwa anahisi kana kwamba nilikuwa nina tabia ya kudeka wakati mimi ni binti wa miaka 10 na aliniona kama mayai .

Kilichoniumiza zaidi ni kuwa hata mwalimu mwenyewe hakuwahi kuniuliza ni kwanini nilikuwa muoga hivyo na hilo liliniumiza mno” asema Jacinta

Mwanadada huyu anasema kuwa maisha yake yalibadilika wakati alipoingia shule ya sekondari kutokana na kuwa alikuwa kwenye shule ya bweni .

Maswali mengi yalikuwa ni kwanini yeye anashindwa kutangamana na wanafunzi wenzake . alizingirwa na wanafunzi wasichana wenzake ambao walikuwa na mori wa maisha hasa kwasababu ndio wakati wanavunja ungo na kuanza kujikubali.

Ila kwake Jacinta maisha yake yalionekana kuwa ya upweke na ya hofu kubwa sana . Anakiri kuwa sio mara moja au mbili amejikuta katika hali ya aibu hasa ilipowadia wakati kuwa lazima angesoma au kutoa hotuba wakati wa masomo mbalimbali.

Hali hiyo ilimwanadama zaidi hata alipojiunga na chuo kikuu. Anakumbuka hafla moja ambayo nusura azimie alipopewa jukumu na muhadhiri wa somo moja kwamba atoe hoja zake mbele ya wanafunzi wenzake .

Jacinta alishindwa kusimama mbele ya watu na badala yake alianza kutokwa na machozi akiomba dunia ipasuke atumbukie ndani.

Jacinta Wambui

“Wakati nimeingia kwenye kampuni mmoja , nikiwa mwanafunzi nilishindwa kutekeleza majukumu yangu ipasavyo, nilikuwa na changamoto ya kutangamana na watu au hata kujieleza .

”Na hapo ndipo niligundua kuwa taaluma niliyoisomea chuo kikuu huenda sitaweza kuitumikia kutokana na hali niliyokuwa naipitia “anasema Jacinta

Mwanzo wa yeye kuchukua hatua za kubadilika , anaitaja kuwa tukio la siku moja mwezi wa Oktoba , na alihisi kuchoka na aina ya hisia alizokuwa anazihisi kila dakika ya maisha yake .Kuanzia shule ya msingi , kuingia sekondari , na hata kwenye taasisi kuelekea ajira yaani alikuwa amefika mwisho .Alianza kutafuta namna ya kusaidika kisaikolojia na kifikra .

”Nikiwa kazini wakati huo nilimpigia shangazi yangu simu na kumueleza kuwa nilikuwa nahitaji msaada wa kisaikoloji, Nilimweleza shangazi kuwa anisaidie kumpata mtaalam wa kutoa nasaha .

”Kipindi hicho nilikuwa ninaathirika sana na hali ya hofu nikiwa kazini” .

Shangazi alimsaidia na kumkutanisha na Mwanasaikolojia mmoja ambaye alianza kutembea naye katika ulimwengu wake wa hofu na uoga usioeleweka

“Wakati ninaanza kumuona mshauri huyo , kitu cha kwanza nilicho jaza kwenye fomu ni kuwa niko hapo kwasababu nilikuwa ninaishi na uoga mwingi na hofu kuu kila wakati , pia nilimweleza kuwa kwa muda nimekuwa nikiwaogopa wavulana na wanaume. Mwanasaikolojia huyo alinieleza kuwa kwa jinsi nilivyokuwa ninalia uchungu wangu ulikuwa unatoka sehemu ya ndani ya moyo wangu “anasema Jacinta.

Mwanadada huyu anasema kuwa alishauriwa pamoja na mambo mengine kuanza kuandika matukio mbalimbali aliyokuwa anahisi kila wakati -Kwa hiyo ilimbidi awe na kitabu maalum cha kuainisha mawazo yake na hisia zake kila wakati .Na ifikapo Jumamosi alikuwa anazuru kwa mtoa nasaha huyo.

“Ila baada ya muda mfupi nilikuwa nahisi kana kwamba sisaidiki katika hali hio ya kupewa nasaha , kwa hiyo baada ya wiki tatu za kwenda kumuona mwanasaikolojia niliacha ghafla maanake niliona kana kwamba fedha nyingi zilikuwa zinatumika na sikusaidika ghafla niliacha kumuona “Jacinta anakumbuka.

Novemba tarehe 6 mwaka wa 2018 aligundua ukweli kuhusu maisha yake , anasema kuwa siku hiyo alikuwa amesalia ofisini peke yake kwani wengi walikuwa kwenye mkutano maalumu nje ya ofisi . Mwanadada huyu anasema kuwa yeye aliendelea kukaa ofisini kutizama video kuhusu ni kwanini yeye huwa na hofu na uoga

Mwanadada huyu anasema kuwa na ugonjwa wa kiakili sio jambo ambalo linakubalika kwa wepesi hasa barani Afrika, na mtu anapojitokeza au kuonesha dalili hizo huwa anabaguliwa , ila ni hali halisi ambayo amepambana nayo kwa miaka -Kukubali kuwa ana ugonjwa wa kiakili ilikuwa ni vita kali maishani mwake .

Jacinta anakiri kubadilika mno akiangalia nyuma akiwa binti wa shule ya sekondari hadi sasa , anasema kuwa amepiga hatua kubwa katika kukabiliana na changamoto za hofu, wasiwasi na uoga mwingi ambao umekuwa sehemu ya maisha yake .

Maoni ya mwanasaikolojia

Kwa sasa Jacinta amerejelea tena matibabu ya kisaikolojia na mshauri mwanasaikolojia wake ni Bi Mercy Ogonda kutoka nchini Kenya . Kama mwanasaikolojia amethibitisha kuwa Jacinta anaishi na hali ya kuwa na wasiwasi na hofu kuu ambayo kiini chake ni matukio ya kuogopesha yaliofanyika utotoni mwake.

Kulingana na mwanasaikolojia huyu ni kuwa Jacinta na watu kama yeye ambao hupitia mateso ,dhuluma za kimwili au za kingono wakiwa watoto wengi huathirika katika siku za utu uzima wao , hasa iwapo hawatapata fursa ya kujadili yaliowatokea wakiwa wadogo .

Kulingana na mwanasaikolojia Bi.Mercy Ogonda mwanasaikolojia kutoka Kenya.

Uoga wa watu (Social phobia) ni uoga uliozidi wa watu au hali ya kijamii. Aliyeathiriwa hudhani atatuhumiwa na kupelelezwa na wengine.

Watu walio na uoga wa watu hutatizika na hufanya lolote wawezalo kuepukana na watu au kuwavumilia. Wao huwa hawafanyi mambo ambayo wangefanya kwa kawaida kwa sababu wapo mbele ya watu.

Watajaribu kujizuia kula, kuongea, kuandika au kunywa kwa njia ya kawaida ama kujitenga na watu.

Je, kuna tiba?

Magonjwa ya wasiwasi yanatibika kikamilifu ingawaje kila ugonjwa au aina ya ugonjwa wa wasiwasi una dalili zake. Magonjwa mengi hutibika kupitia matibabu ya kisaikolojia au dawa.

Matibabu yanayotumia mbinu za kisaikolojia pamoja na dawa huwa na matokeo bora yanayodumu. Matibabu kamili ya anxiety disorder ni kama;

• Mbinu za kisaikolojia kama urekebishaji wa tabia (Cognitive Behavioural Therapy CBT) zinazolenga kubadilisha mawazo, tabia na imani zinazoleta wasiwasi. Mbinu hizi zaweza pia kumfanya aliyeathiriwa kupitia yale mambo yanayosababisha wasiwasi (yaani desensitization).

• Mbinu za kupunguza wasiwasi na kutulia.

• Dawa zinazopunguza huzuni ni muhimu katika kutibu wasiwasi fulani na pia kutibu huzuni.

• Dawa ya wasiwasi inayolenga akili pia ni muhimu

• Madawa hayatatibu wasiwasi lakini hupunguza dalili za ugonjwa huu mtu apatapo matibabu ya kisaikolojia. Jamii na marafiki wa watu walio na wasiwasi mara nyingi hutatizika. Usaidizi na elimu ni muhimu kwa kutibu ugonjwa huu.